JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limekamata jumla ya watuhumiwa 227 kwa makosa mbalimbali katika operesheni zilizofanyika kati ya 12 Mei na 8 Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Gallus Hyera watuhumiwa 107 walikamatwa wakiwa na mali mbalimbali zinazodaiwa kuwa za wizi pamoja na dawa za kulevya. Miongoni mwa vitu vilivyokamatwa ni pamoja na kilo 52 za mirungi, kilo 3.5 za bangi, lita 300 za pombe ya moshi, televisheni 18, simu za mkononi, pikipiki 21, vifaa vya majumbani na nyara za serikali zikiwemo ngozi 12 za twiga na pembe tatu za tandala.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa watuhumiwa 50 walikamatwa kwa tuhuma za uporaji wa kutumia pikipiki maarufu kama “vishandu”, huku wengine 15 wakikamatwa kwa makosa yanayohusisha matumizi ya silaha na watuhumiwa 14 kwa biashara ya ukahaba.
Aidha, raia sita wa kigeni walikamatwa kwa kuingia nchini bila vibali halali na kukabidhiwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi za kisheria.
Kwa upande wa usalama barabarani, Polisi walikamata makosa 11,725 ya usalama wa barabarani yaliyotozwa faini, huku madereva wawili wa mabasi wakifutiwa leseni kutokana na makosa ya mwendokasi, ulevi na kusababisha ajali.
Katika hatua nyingine, Mahakama imetoa hukumu kwa baadhi ya kesi zilizowasilishwa ambapo mtuhumiwa mmoja wa ubakaji amehukumiwa kifungo cha miaka 30, mmoja wa kujeruhi amehukumiwa miaka mitano jela pamoja na kulipa fidia ya Sh. 500,000, watuhumiwa wanne wa kubaka kwa kundi wamehukumiwa kifungo cha maisha, na wanane waliopatikana na hatia ya biashara ya ukahaba wamehukumiwa kifungo cha miezi minne jela.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na kufika vituo vya polisi kutambua mali zinazodhaniwa kuibwa kwa kuwasilisha vielelezo vya umiliki.