MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi imewahukumu watu wawili vifungo vya muda mrefu gerezani katika kesi mbili tofauti za ubakaji wa mtoto na umiliki haramu wa nyara za serikali, baada ya kupatikana na hatia ya makosa hayo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Lindi … (endelea).
Katika kesi ya ubakaji, mshtakiwa Hamis Rashid Mkon’gonda (55), amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani pamoja na kulipa fidia ya shilingi milioni moja baada ya kutiwa hatiani kwa kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Consolata Singano baada ya mahakama kujiridhisha kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote.
Katika kesi nyingine, Michael Atanas Antoni (46), amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki vipande vitatu vya nyama ya mnyama aina ya ngiri bila kibali halali kutoka mamlaka husika.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Khalfan Omari Khalfan, huku pande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Jordan Kyambo.