JUMLA ya vijana 588 wameanza rasmi mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA Kihonda (Morogoro) na VETA Mwanza kupitia mpango wa NBC Wajibika Scholarship, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya NBC na VETA. Anaripoti Mwandishi WEtu, Dar es Salaam … (endelea).
Kupitia mpango huu, NBC imetoa zaidi ya Sh. 150 milioni kugharamia mafunzo katika fani za ufundi umeme, ufundi bomba, pamoja na ubunifu, ushonaji na teknolojia ya nguo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa NBC, Godwin Semunyu, alisema uwekezaji huo unalenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri, kuajiriwa na kuwaajiri wengine, huku ukichangia ukuaji wa uchumi jumuishi nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, John Mwanja, aliipongeza NBC kwa mchango wake katika kuendeleza elimu ya ufundi stadi, huku Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda, Dk. Ulimwengu Salumu, akibainisha kuwa mafunzo hayo ya miezi mitano yanajumuisha nadharia, vitendo, ujasiriamali na stadi za maisha.
Wanufaika wa mpango huo wameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutimiza ndoto zao za kujitegemea kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii.