Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA), Bw. Abel Uronu, ameweka wazi kuwa mageuzi makubwa ya teknolojia ya meli duniani yanailazimisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa, na uwekezaji huo hauwezi kukamilika bila kuwepo kwa Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID).Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza mkoani Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa tozo hiyo ambayo hivi karibuni TPA iliishusha kutoka asilimia 9% hadi 4.5% ya kodi ya forodha baada ya kusikiliza wadau, Uronu amefafanua kuwa tozo hii inakwenda kuzaa miradi mikubwa ya kimkakati itakayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye bandari za kisasa.
Uronu ametolea mfano maendeleo katika bandari kubwa duniani ambako kazi zote zinaendeshwa kwa mifumo ya kielektroniki na kidijitali, hakuna misongamano ya watu wala malori.
“Tanzania tuna MGR, SGR na pia tuna TAZARA. Sasa hizi zote zinatakiwa ziwe zinapokea mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo kuna maendeleo ambayo kwa njia moja au nyingine TPA wanahusika. Haya maendeleo sasa hayawezi kufanyika kama TPA haitakusanya hizi tozo kwa sehemu”, amesema Abel Uronu.