CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Jumatano 20 Mei 2026 kimewasilisha baruapepe kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kujibu sharti lililotolewa na Ofisi hiyo lililokitaka chama hicho kueleza sababu za kutosimamishiwa usajili wake kutokana na madai ya kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na matamshi ya viongozi wake yanayodaiwa kuhatarisha amani, usalama na utulivu wa nchi.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Hatua hiyo inakuja baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia barua ya 7 Mei 2026 kueleza kuwa Ofisi yake imekuwa ikifuatilia mwenendo wa viongozi wa Chadema kupitia mikutano ya hadhara, taarifa za vikao vya chama hicho pamoja na maudhui yanayosambazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Katika barua hiyo, Msajili alikipa chama hicho muda wa wiki mbili kuwasilisha maelezo ya kwanini kisichukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Miongoni mwa hoja zilizotajwa na Ofisi ya Msajili ni kauli zinazodaiwa kutolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kuhusu mpango wa kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kuachiwa kwa mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu.
Kwa mujibu wa Msajili, kauli hizo zinaweza kutafsiriwa kama kuchochea taharuki, migogoro ya kisiasa pamoja na kuingilia mwenendo wa shauri ambalo bado linaendelea mahakamani.
Kwa miaka kadhaa sasa, uhusiano kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Chadema umekuwa ukikumbwa na mvutano wa mara kwa mara, huku hatua mbalimbali za kinidhamu, onyo na barua zikielekezwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani.
Hali hiyo imeendelea kuibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania. Wakati baadhi ya wadau wakiona hatua hizo ni utekelezaji wa sheria na usimamizi wa nidhamu ya vyama vya siasa, wengine wamekuwa wakizitafsiri kama mwendelezo wa kuandamwa kwa upinzani, hususan Chadema