CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema madai ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba kauli za Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, zina uchochezi na kuhatarisha usalama wa nchi hayana msingi wa kisheria.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kupitia barua yake ya leo Jumatano 20 Mei 2026, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, chama hicho kimesema tafsiri iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haiendani na misingi ya demokrasia ya vyama vingi na inakiuka mamlaka ya Mahakama katika kuamua kesi za aina hiyo.
Barua hiyo ilikuwa ni majibu kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyoitaka Chadema kueleza sababu za kutosimamishiwa usajili wake kwa madai ya kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na kuhatarisha amani pamoja na usalama wa nchi.
Kwa mujibu wa Msajili, matamshi ya Heche kuhusu uwezekano wa wananchi kufanya maandamano kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, yalidaiwa kuhatarisha amani na usalama wa nchi kwa mujibu wa Kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Hata hivyo, Chadema imesema kauli ya kisiasa inayozungumzia maandamano ya amani haiwezi kufasiriwa kama uchochezi wa vurugu, ikisisitiza kuwa maandamano ya amani ni haki halali inayotambulika kitaifa na kimataifa katika mfumo wa kidemokrasia.
“Kauli ya kisiasa inayozungumzia maandamano ya amani si sawa na uchochezi wa vurugu. Katika mazingira ya kidemokrasia, maandamano ya amani ni nyenzo halali ya kisiasa inayotambulika kitaifa na kimataifa,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Chama hicho pia kimesema hakuna sehemu ambayo Heche alihamasisha wananchi kufanya vurugu, kutumia nguvu, kufanya uharibifu au kuivamia Mahakama.
Aidha, Chadema kimesisitiza kuwa kesi inayomkabili Lissu ni ya kisiasa, huku kikieleza kuwa kuhoji mwenendo wa mashauri yenye maslahi ya umma au kutoa maoni kuhusu utendaji wa dola si kosa la jinai wala ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Mnyika amesema uhuru wa Mahakama haulindwi kwa kuwanyamazisha wananchi au vyama vya siasa, bali kwa Mahakama kutenda haki kwa mujibu wa sheria bila kuingiliwa.