CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuzikataa tuhuma zilizotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kikisema hakijakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa bali kimekuwa kikitekeleza haki za kisiasa na Kikatiba zinazolindwa na Katiba ya Tanzania.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Katika barua iliyotumwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa leo 20 Mei 2026, na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika amesema Chadema kimesisitiza kuwa hakitakubali kunyimwa haki zake za kisiasa na kiko tayari kutumia njia zote halali za kisheria, Kikatiba na Kidemokrasia kulinda uhuru wa chama pamoja na wanachama wake.
Chama hicho kimeeleza kuwa hakijatenda kosa lolote linalostahili adhabu ya kusimamishwa usajili au kutozwa faini, kikidai kuwa kimekuwa kikifanya shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria na uwajibikaji.
Katika maelezo yake, Chadema pia kimekosoa kile kilichokiita uchunguzi wa “kimaigizo” kuhusu matukio ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, kikisema hakipo tayari kuona wananchi wakisahaulishwa kuhusu matukio hayo.
Aidha, chama hicho kimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba ya Tanzania pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu ikiwemo Agano la Afrika la Haki za Binadamu na Watu la mwaka 1981 na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 1999.
Chadema pia kimesema kifungu cha 19(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ni kinyume cha Katiba, kikieleza kuwa madai yote yanayotolewa dhidi yake yanapaswa kusikilizwa na Mahakama pekee kwani yanahusu tuhuma za jinai.
Sambamba na hilo, chama hicho kimesisitiza kuwa kupinga mfumo mbovu wa uchaguzi na kukemea wizi wa kura ni sehemu ya uzalendo na kulinda misingi ya demokrasia nchini.