RAIA wa Kenya, Rachel Wandeto, ambaye alipata umaarufu mitandaoni kwa kuchora tattoo yenye sura ya Rais wa Kenya, William Ruto, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Taarifa kutoka hospitali zinasema Wandeto alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kenyatta jijini Nairobi kutokana na majeraha makubwa aliyopata baada ya tukio lililoripotiwa kutokea eneo la Mwiki, Kasarani.
Inadaiwa kuwa alishambuliwa kwa kumwagiwa petroli kabla ya kuwashwa moto, tukio lililomuacha na majeraha ya moto yanayokadiriwa kufikia asilimia 70 ya mwili wake. Awali alipelekwa katika Hospitali ya Uzima Uhai kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta kwa ajili ya matibabu maalum huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Rachel Wandeto, ambaye pia alikuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, alikuwa amejipatia umaarufu mkubwa mtandaoni kutokana na picha na video zake zikimuonesha akiwa na tattoo ya Rais Ruto pamoja na ujumbe wa kumuunga mkono kisiasa.
Tukio hilo limezua mshtuko nchini Kenya na kuibua mjadala kuhusu ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake pamoja na athari za siasa na mitandao ya kijamii katika maisha ya watu.