MWANASIASA na Katibu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amedai kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inachochea migogoro ndani ya vyama vya upinzani nchini.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza na Mwanahalisi Digital, Sheikh Ponda amedai kuwa ofisi hiyo inachochea migogoro hiyo kwa kuingilia baadhi ya mambo yanayopaswa kutekelezwa kwa uhuru na vyama hivyo.
Amesema kuwa ili kuondoa changamoto hiyo ni muhimu kuwepo kwa sheria zitakazovifanya vyama vya siasa kuwa huru, imara na visivyoingiliwa katika shughuli zake za ndani.
Sheikh Ponda mfumo wa kisheria unaolinda uhuru wa vyama vya siasa utasaidia kupunguza migogoro ya mara kwa mara na kuimarisha demokrasia nchini.
Aidha, amevitaka vyama vya upinzani kuacha kulaumiana na badala yake kushikamana ili kujenga nguvu ya pamoja yenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini.
Kauli za Sheikh Ponda zinakuja wakati baadhi ya vyama vya upinzani vikiendelea kukumbwa na migogoro ya ndani kuhusu uongozi na uendeshaji wa shughuli zao.