KESHO 9 Julai 2026, macho ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla yataelekezwa Ikulu Zanzibar ambako kutafanyika Hafla ya Uwasilishaji wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa, tukio linalotarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamano, amani na ustawi wa kisiasa visiwani humo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Hafla hiyo itakayofanyika kuanzia saa 4:00 asubuhi katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, itaongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Mwinyi, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman. Viongozi hao wanatarajiwa kuwasilisha rasmi tamko la Pamoja la muafaka wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.
Mbali na uzinduzi wa tamko hilo, viongozi hao wataeleza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa ajenda mbalimbali zilizokubaliwa na pande zote mbili, zikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kujenga mazingira ya utulivu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali na wanahabari, hali inayoonesha uzito wa tukio hilo katika mwelekeo wa kisiasa wa Zanzibar.
Aidha, wananchi watapata fursa ya kufuatilia hafla hiyo mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa, huku matarajio yakiwa ni kuona tamko hilo likiendelea kuwa msingi wa kudumisha maridhiano, amani na maendeleo endelevu nchini Zanzibar.