MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Said Mzee Said, ameliomba Jeshi la Polisi kuwaachia huru makada sita wa chama hicho wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano yanayodaiwa kufanyika 7 Julai 2026.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza katika Kata ya Chinongwe mkoani Lindi leo19 Juni 2026, Mzee amesema Chadema haihusiki na maandamano hayo kama inavyodhaniwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Amesema amepokea taarifa za kukamatwa kwa makada hao sita kwa madai ya kuhamasisha maandamano hayo, huku akisisitiza kuwa chama chake hakina mpango wala maandalizi yoyote ya kuandaa maandamano hayo.
“Nimearifiwa kuwa kuna makada wetu sita wamekamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano. Nataka niwathibitishie wananchi wa Chinongwe na Watanzania wote kwa ujumla kwamba Chadema haiandai maandamano ya tarehe 7 Julai 2026. Hayo si maandamano yetu,” amesema Mzee.
Aidha, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo ili kubaini wahusika halisi badala ya kuwahusisha wanachama wa Chadema bila ushahidi wa kutosha.
Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na taarifa za maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika 7 Julai 2026, huku vyombo vya usalama vikiendelea kufuatilia taarifa mbalimbali zinazohusiana na tukio hilo