RAIS wa Kenya, William Ruto, amesema kuwa serikali haitavumilia vitendo vya vurugu, uharibifu wa mali na machafuko wakati baadhi ya vijana wa nchi hiyo wakitangaza kufanya maandamano Juni 25 wiki ijayo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Mpango huo wa baadhi ya vijana wa Kenya ni maadhimisho ya kumbukumbu ya maandamano yaliyofanyika 25 Juni 2024 nchini humo ambapo maelfu ya vijana maarufu ‘Gen Z’ walifanya maandamano ya kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 (Finance Bill 2024).
Wakati huo waandamanaji waliingia ndani ya viunga vya Bunge jijini Nairobi baada ya wabunge kupitisha muswada huo waliodai una utata.
Akizungumza leo Ijumaa 19 Juni 2026 katika mkutano wa kitaifa wa utendaji na uzalishaji uliofanyika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema Kenya itaendelea kulinda haki za wananchi za kuandamana, lakini akasisitiza uhuru huo haupaswi kutumiwa kuhatarisha utulivu, uchumi na maendeleo ya nchi.
“Kenya ni taifa linaloamini kwa dhati katika utaratibu, sisi ni taifa lililostaarabika, jamii iliyopangika na tunaamini katika utawala wa sheria,” amesema Ruto.
Rais huyo ameeleza kuwa kila mwananchi ana haki ya kuwasilisha malalamiko yake au kuandamana kwa mujibu wa sheria, huku Serikali ikiwa na wajibu wa kulinda haki hizo.