SERIKALI imesema hadi sasa Tanzania haina mgonjwa wa Ebola na imesisitiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kuwalinda wananchi wake.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo, kutokana na mlipuko unaoendelea kuripotiwa katika nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika taarifa yake Waziri amesema hadi kufikia18 Juni 2026, Tanzania haikuwa na mgonjwa wa Ebola aliyeripotiwa nchini na hali ya usalama wa afya inaendelea kuwa nzuri.
“Napenda kuwafahamisha wananchi kuwa hadi sasa nchi yetu haina mgonjwa wa Ebola na Serikali imejipanga kikamilifu kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti tishio lolote linaloweza kuhatarisha afya za Watanzania,” amesema Mchengerwa.
Kwa mujibu wa Waziri, tangu kutangazwa kwa tishio hilo, tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa na kufanyiwa uchunguzi ambapo wahisiwa 11 walikidhi vigezo vya uchunguzi na kuchukuliwa sampuli zilizothibitisha kutokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.
Amesema hatua zote muhimu zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na wataalamu wa afya hapa unakuwa wa hali ya juu ili kulinda na kuzuia ugonjwa huo.