KAMATI ya Mahusiano ya Nje ya Seneti ya Marekani imepitisha muswada unaotaka kufanyika kwa tathmini ya kina ya uhusiano kati ya Marekani na Tanzania kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni ongezeko la matukio ya vurugu za kisiasa na kudorora kwa misingi ya demokrasia nchini Tanzania.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Muswada huo wa pande mbili za kisiasa umeandaliwa na Seneta wa chama cha Democratic, Jeanne Shaheen, kwa kushirikiana na Seneta wa chama cha Republican, Ted Cruz.
Kwa mujibu wa muswada huo, Serikali ya Marekani itaelekezwa kufanya mapitio ya kina ya ushirikiano wake na Tanzania pamoja na kutathmini athari za mwenendo wa kisiasa wa nchi hiyo kwa maslahi ya Marekani katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Sehemu ya muswada huo imeeleza kuwa tathmini hiyo pia itachunguza kwa kina uhusiano unaokua kati ya Tanzania na mataifa ya China na Russia, pamoja na kupima athari zake kwa maslahi ya kimkakati na kiuchumi ya Marekani katika eneo hilo.
Akizungumza baada ya kamati hiyo kupitisha miswada mbalimbali ya sera za nje, Seneta Shaheen alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Kamati ya Mahusiano ya Nje ya Seneti katika kuimarisha uongozi wa Marekani duniani, kulinda usalama wa taifa na kuhakikisha sera za nje zinawanufaisha wananchi wa Marekani.
Iwapo muswada huo utapitishwa na Bunge la Marekani na kutiwa saini kuwa sheria, utailazimu Serikali ya Marekani kuwasilisha tathmini rasmi kuhusu hali ya uhusiano wake na Tanzania pamoja na mwelekeo wa kisiasa na kidiplomasia wa nchi hiyo katika mazingira ya ushindani wa kimataifa unaohusisha mataifa makubwa duniani.
Maamuzi hayo yamefikiwa 17 Juni 2026 wakati Kamati ya Mahusiano ya Nje ya Seneti ya Marekani ilipokutana na kupitisha miswada kadhaa ya sera za nje, ikiwemo muswada wa Reassessing the United States–Tanzania Bilateral Relationship Act unaohusu uhusiano kati ya Marekani na Tanzania.