WAANDAAJI wa mbio za Absa Dar City Marathon 2026 kwa kushirikiana na The Runners Club wametoa vifaa tiba kwa kliniki ya wajawazito katika Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya nchini. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo leo, waandaaji hao walisema msaada huo ni mwendelezo wa mchango wao kwa hospitali hiyo, ambapo kwa miaka mitatu mfululizo wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali yenye lengo la kusaidia kupunguza changamoto zinazoikabili taasisi hiyo ya afya.
Walieleza kuwa Hospitali ya Mnazi Mmoja ni miongoni mwa vituo vya afya vinavyopokea idadi kubwa ya wagonjwa, hususan wajawazito na watoto, jambo linaloongeza mahitaji ya vifaa tiba na huduma bora za afya.
Kwa mujibu wa hospitali hiyo, zaidi ya wajawazito 200 hupokelewa katika wodi ya wazazi huku zaidi ya watoto 400 wakihudumiwa kila siku katika kliniki ya afya ya uzazi na mtoto. Hali hiyo imeifanya hospitali kuendelea kuhitaji ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuboresha utoaji wa huduma.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilienda sambamba na kampeni ya uchangiaji damu iliyoandaliwa na The Runners Club kwa kushirikiana na wadhamini wa marathon, washirika, wauzaji, watoa huduma na wananchi kwa ujumla.
Msaada huo ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazotekelezwa na Absa Dar City Marathon na The Runners Club, zinazolenga kuchangia maendeleo ya sekta ya afya na ustawi wa jamii.