TUME ya kuchunguza jinai kwenye matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025, ‘tume ya Jaji Lila inawakati mgumu wa utekelezaji wa majukumu yake kutokana na kutokubalika kwake. Anaripoti Mwandishi Wetu Dar es Salaam …(endelea).
Vyama vya upinzani na wanaharakati nchini inapinga tume hiyo kufanya majukumu ya uchunguzi kwa kueleza kuwa haina sifa kikatiba wala kisheria ya kufanya kazi iliyopangiwa kufanya.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Shabani Lila, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Wanaharakati wameipinga tume hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, wakipinga uhalali kuundwa kwa tume hiyo .
Waombaji kwenye shauri hilo ni pamoja na Buberwa Ephraim Kaiza na mwenzake Joseph Daud Mabugo.
Isihaka Mchinjita, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo – Bara amesema kuwa tume hiyo msingi wake ni Tume ya Jaji Chande ambayo haikulisaidia taifa kujinasua na mkwamo uliokuwepo.

Sisi kama ACT Wazalendo tangu awali tuliikata ile Tume ya Jaji Chande na tukasema haina uwezo wa kutupatia kinachotakiwa kwa maana ya kutoa matokeo ambayo yataisaidia nchi
Amesema kuwa Kwenye tume ya Jaji Chande ACT ilijenga hoja kwenye aina ya watu waliounda tume na nani anapokea ripoti
Kuhusu Tume ya Jaji Lila amesema kuwa tume hiyo sio ya kuitegemea.
“Ninachoweza kusema ni kwamba ni kitu ambacho huwezi kukipa mategemeo makubwa kwa sababu ni kama shauri lililokuja vibaya mahakamani huwezi tegemea kwamba jaji atakaye lihukumu hilo shauri ataweza kuliweka vizuri yaani ripoti ya Jaji Chande ilishindwa kwa sehemu kubwa sana kutuonyesha maeneo ambayo ilikuwa na maswali yasiyojibika.
Amesema msingi wa tume hiyo ni ripoti hiyo anayoitaja kuwa imefeli .
“Sehemu kubwa ilijielekeza kwenye kuonesha mapungufu ya wale walioandamana ikiwa kwenye sheria mauaji ni kosa kubwa na ni kawaida kosa kubwa kuyafuta makosa madogo”
Amesema kuwa Ripoti ile haijaeleza nani alitoa amri ya raia kuawa hata hadidu za rejea walizopewa zilikuwa haziwataki waende huko.
“Sipati matumaini na Tume hii kama inaweza kutegemewa kulisaidia taifa letu’
Wakili wa Mahakama Kuu, Peter Madeleka, amesema kuwa pamoja na Rais kuwa na mamlaka ya kuunda tume za uchunguzi lakini kazi iliyopewa tume hiyo limepokwa jeshi la polisi majukumu yake yake ya kisheria.

“Tunayo sheria ni kifungu cha 12 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ambayo ni sura ya 20 ya sheria za Tanzania, hicho kifungo kimetoa mamlaka kwa jeshi la polisi kupeleleza jinai zote, wakati wote jinai inapotekea kwa hiyo kama tunakubali Oktoba 29 kuna jinai ilifanyika ya watu kuuliwa pasipokufuata sheria huo ndio wajibu wa jeshi la polisi ambao tunashangaa kwanini mpaka sasa haujatekelezwa mpaka ikapelekea tume kuundwa.
Madeleka amesema kuhusu kuunndwa kwa tume itakayoanzisha mchakato wa watu kushtakiwa anasema ni mkanganyiko kwa sababu tayari vijana kadhaa walishakamatwa na kushtakiwa kwa uhaini.
“Ni Mkanganyiko kwa sababu tayari polisi walishatekeleza hilo jukumu mapema kabisa ndani ya siku kadhaa baada ya matukio yake kufanyika , watu walikamatwa na polisi upelelezi wa jinai ukafanyika, tukagundua kosa walililofanya ni uhaini, wale watu wakafikishwa mahakamani kwa mamlaka ya DPP, wakashtakiwa na baaadaye DPP huyo huyo akawaachia na Rais akasema kuachiwa kwa watu wale kulitokana na falsafa 4R ya Rais Mwenyewe kwamba hawa watu waachiwe walifuata mkumbo hata kama walifanya uhaini uliopelekea watu kuuliwa sasa leo unapounda tume ya Jaji Lila kuja kuchunguza jinai, jinai gani tena, unamchunguza nani, kwa sababu waliofanya hiyo jinai tunawajua kwa majina yao na walipelekwa mahakamani, na rekodi zipo mahakamani”
“Sielewi tunatoka wapi tunaelekea wapi kuhusu suala la 29 oktaba kwa sababu tayari sisi tunawajua watu waliofanya yale mauaji na tunawajua kupitia serikali kwa mamlaka rasmi kabisa kwa maana ya Polisi, DPP na mahakama,”. Alisema Madeleka
Dk. Khamis Masoud, Mkurugenzi wa kituo cha usaidizi wa kisheria nchini ELAF, amesema kuwa shida sio tume shida ni walihusika na matukio ya Oktaba 29 kuwajibika na kuwajibishwa.
“Maofisa wa vyombo vya dola walitakiwa kujiuzulu kwani tendo hilo lingekuwa ni la kizalendo kwa sababu ya kushindwa kutekeleza wajibu wao”
Dk. Masoud ameongeza “Hata ripoti ya Jaji Chande ilieleza jinsi makazi ya wahalifu waliotekeleza yale yalivyokuwa karibu na vituo vya polisi hii ni wazi kuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao”
Amesema kuwa sababu za matukio hayo ni malalamiko ya muda mrefu ya mifumo ya uchaguzi lakini na watu kupotea hili lipo wazi halihitaji kuundwa tume.