MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ameikosoa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akiituhumu kuendesha kile alichokiita kampeni ya kukihujumu chama hicho kupitia mfululizo wa barua za onyo zinazotolewa baada ya mikutano ya hadhara.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kauli hiyo imefuatia barua ya 26 Mei 2026 iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, inayokitaka Chadema kutoa maelezo ifikapo 8 Juni 2026 kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa sheria, huku chama kikikabiliwa na uwezekano wa kufutiwa usajili au kutozwa faini chini ya marekebisho ya Sheria Namba 3 ya Mwaka 2024.
Kupitia mitandao ya kijamii, Heche alidai kuwa Ofisi ya Msajili imekuwa ikiifuatilia Chadema kwa karibu na kwamba viongozi wa chama hicho huandikiwa barua kila wanapotoa kauli za kisiasa.
Aidha, alimhusisha Nyahoza na kesi ya mgawanyo wa mali iliyokuwa imekifungia chama kufanya shughuli zake kabla ya mahakama kuifuta hivi karibuni.
Katika barua hiyo mpya, Ofisi ya Msajili imeeleza kuwa imepokea na kuchambua video tatu zinazosambaa mtandaoni zikionyesha baadhi ya viongozi wa Chadema wakitumia lugha iliyotajwa kuwa isiyofaa kwa viongozi wa kisiasa.
Akijibu hoja za Chadema kuwa hatua hiyo inakiuka amri ya mahakama iliyotolewa hivi karibuni, Nyahoza alisema zuio hilo lilihusu barua ya awali ya 7 Mei pekee na halizuii ofisi yake kuchukua hatua kuhusu matukio mapya yanayodaiwa kukiuka sheria.
Nyahoza amesisitiza kuwa jukumu la Ofisi ya Msajili ni kusimamia utekelezaji wa sheria na maadili ya vyama vya siasa, akiwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za kujenga siasa za kistaarabu zinazozingatia hoja badala ya matumizi ya lugha za matusi katika majukwaa ya kisiasa.