UMOJA wa wanawake kutoka vyama 12 vya siasa nchini Tanzania umeitaka Serikali kuunda tume maalum ya uchunguzi kuhusu matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea kujitokeza nchini, huku wakisisitiza kuwa wahusika wakibainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo 26 Mei 2026, Mwenyekiti wa Wanawake Taifa wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Rachel Balama amesema kuwa ni muhimu Serikali kuongeza juhudi za kuimarisha usalama wa wananchi ili kukabiliana na vitendo hivyo vinavyozua hofu kwa jamii.
Amesema miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni pamoja na kufungwa kwa kamera za CCTV katika maeneo muhimu ya mijini pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia za kiusalama ili kuwabaini wahalifu kwa haraka kabla na baada ya matukio ya uhalifu kutokea.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chama cha NLD Taifa, Mwajuma Mirambo amesema Serikali inapaswa kuongeza jitihada za makusudi katika kuboresha afya ya mama na mtoto, akieleza kuwa bado kuna changamoto kubwa katika sekta hiyo inayohitaji ufumbuzi wa haraka.
Naye Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha DP, Rehema Shauri amesema wanawake wana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi kwa kuwa wao ndio walezi wakuu wa familia na msingi wa malezi katika jamii.
Vyama hivyo 12 vya siasa nchini ni Tanzania Labour Party (TLP),Chama cha Kijamii(CCK),Chama cha Demokrasia(DP),National Reconstruction Alliance(NRA),Sauti ya Umma(SAU),UMD,United Democratic Party(UDP),NCCR-Mageuzi,AAFP,ADA TADEA,Chama cha Demokrasia MAKINI na UPDP.