MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Melikisedeki Kaijage, anakabiliwa na mashtaka mazito ya uhujumu uchumi na ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, akituhumiwa kupanga njama za kuchoma moto majengo yote ya umma nchini pamoja na makazi ya askari polisi.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
​Akizungumza jijini Dodoma jana 19 Agosti 2026, Wakili wa Kujitegemea, Godfrey Wasonga, amebainisha kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 16278/2026, lenye makosa mawili yaliyowekwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Siku Nyingi.
​Wakili Wasonga ameeleza kuwa kulingana na hati ya mashtaka, Dk. Kaijage anatuhumiwa kutenda makosa hayo mnamo 3 Julai 2026 akiwa katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa kupanga mikakati ya kuchoma majengo ya umma kuanzia ngazi ya vitongoji, shule, vituo vya afya, mahakama, makazi ya polisi, hadi Ikulu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mtuhumiwa anatuhumiwa kwamba alikuwa na matarajio ya kuchoma majengo yote ya umma yaliyoko Tanzania kuanzia vitongoji, shule, hadi Ikulu, pamoja na makazi yote ya askari polisi Tanzania Bara na Zanzibar. Mtu mmoja anatuhumiwa kupanga hayo yote,” amesema Wakili Wasonga.
​Kuhusu mwenendo wa shauri hilo, Wakili Wasonga ameeleza kuwa kesi hiyo ilipangwa kuendelea kwa hatua ya Uchunguzi wa Awali (Preliminary Inquiry) ili kujiridhisha kabla ya kumhamishia mshtakiwa Mahakama Kuu, lakini ilishindwa kuendelea kutokana na Hakimu Mkazi anayeendesha shauri hilo,Zabibu Mpangule, kutokuwepo mahakamani.
​Shauri hilo lilihairishwa na Hakimu Mkazi Kombe hadi tarehe 27 Agosti 2026 litakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa. Kwa kuwa makosa ya kigaidi na uhujumu uchumi hayana dhamana kisheria, Dk. Kaijage anaendelea kushikiliwa mahabusu.
​Ikumbukwe kuwa mnamo 21 Julai 2026, Dk. Kaijage alikuwa amepewa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kufuatia kushikiliwa kwake katika Kituo cha Polisi Chang’ombe tangu 8 Julai 2026, lakini kabla ya kutekeleza masharti ya kuachiwa, alikamatwa tena na kufunguliwa mashtaka hayo mapya.