WAKILI Peter Madeleka amekanusha vikali tuhuma zinazomkabili kutoka Jeshi la Polisi za kudharau amri ya Mahakama, akisema hatambui wala hakumbuki kuwepo kwa amri yoyote ya Mahakama anayodaiwa kuivunja.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Madeleka ametoa kauli hiyo leo 18 Agosti 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari akiwa ameambatana na viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), akisisitiza kuwa tuhuma hizo hazina msingi wa kisheria na kwamba zinalenga kumkandamiza.
Kwa mujibu wa Madeleka, alikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) tangu 14 Agosti 2026, kabla ya kuhamishwa usiku wa manane chini ya ulinzi mkali kwenda Kituo cha Polisi Mbweni bila kupewa sababu za msingi.
Alisema baadaye alirejeshwa Kituo Kikuu cha Polisi na kupewa dhamana 17 Agosti 2026.
“Sitambui kama kuna amri yoyote ya Mahakama iliyotolewa au ambayo nimeichukua na kuidharau kama inavyodaiwa,” alisema Madeleka.
Aliongeza kuwa hata kama amri hiyo ipo, kwa mtazamo wake, kosa la kudharau Mahakama chini ya Kifungu cha 114 cha Kanuni ya Adhabu linapaswa kushughulikiwa mbele ya Mahakama iliyodaiwa kudharauliwa, badala ya kuwa suala la upelelezi wa Polisi.
Madeleka alitoa kauli hiyo baada ya kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya masharti ya dhamana aliyopewa.
Katika hatua nyingine, Madeleka alikishukuru Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kupitia Mwenyekiti wa Mawakili Vijana (YAL), Wakili Emmanuel Okashu, kwa kufika kwa wakati na kumpatia msaada wa kisheria wakati wote wa kipindi alichokuwa akikabiliwa na tuhuma hizo.
Taarifa za Madeleka zinakuja wakati suala la madai ya kudharau amri ya Mahakama likiwa limeibua mjadala kuhusu namna masuala ya aina hiyo yanavyopaswa kushughulikiwa kisheria