Rais Samia Suluhu Hassan, amehitimisha rasmi Tamasha la Kizimkazi na kuwashukuru wadau mbalimbali, ikiwemo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa mchango wao katika kufanikisha tamasha hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
NBC ilishiriki katika Maonyesho ya Biashara na kudhamini hafla maalum ya mnada wa sanaa za picha iliyoongozwa na Rais Samia, iliyolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alitoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zilizopo Kizimkazi, akisema maendeleo ya miundombinu na miradi mbalimbali yameongeza mvuto wa eneo hilo kwa biashara na uwekezaji.
“Wilaya ya Kusini imepata mabadiliko makubwa sana ikilinganishwa na mwaka 2016 kutokana na kuongezeka kwa fursa za biashara zilizotokana na uwekezaji, hususani kwenye maeneo ya utalii… Tunawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hizi,” alisema.
Akizungumzia wito huo wa Rais Samia, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema benki hiyo imejipanga kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kupata mitaji na huduma mbalimbali za kifedha ili kukuza biashara na kuchochea uchumi wa Kizimkazi na Zanzibar kwa ujumla.
“Ushiriki wa NBC katika Tamasha la Kizimkazi kwa takribani miaka sita mfululizo unaakisi dhamira yetu ya kuwa karibu na jamii, wafanyabiashara na wawekezaji, huku tukiunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi, uwekezaji na maendeleo endelevu.’’ Alisema Sabi.