CHUO kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanza kufanya utafiti wa kumtumia panya kubaini nyara za serikali na tayari majaribio yameshaanza ili kukabiliana na suala la ujangili hapa nchini. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).
Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Raphael Chibunda amesema hayo leo wakati Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alipotembelea banda la SUA kwenye maonesho ya 88 Kanda ya Mashariki.
Chibunda amesema SUA imeanzisha mradi huo mpya unaolenga kukabiliana na changamoto ya ujangili kwa kuwatumia panya buku kubaini nyara za serikali na kwamba panya hao tayari wameshaanza kutumika kwa majaribio katika maeneo ya viwanja vya ndege na bandarini.
Mtafiti kutoka kituo cha kudhibiti wanyama waharibifu wa mazao (PEST- Management) SUA Princus Mramba amesema mradi huo umeanza miaka minne iliyopita ambapo kwa sasa panya hao wamepelekwa nchini Uturuki ili kubaini watu waliofukiwa kwenye vifusi.
Mramba amesema panya hao baada ya kumaliza mafunzo watatumika na Sekta za kiserikali za wanyamapori ambazo zitaingia mikataba na taasisi zitakazohitaji kuwatumia kama vile bandari na viwanja vya ndege.
Wakati huo huo Prof. Chibunda amesema SUA pia wameanzisha utafiti wa kutumia bundi kudhibiti panya mashambani.
Amesema kulingana na utafiti aliofanya bundi moja anauwezo wa kula panya 15 kwa siku hatua ambayo inaweza kudhibiti wadudu hao waharibifu wa mazao kwenye mashamba.
Hata hivyo Chibunda amesema pia SUA ina hospitali ya Rufaa ya kutibu wanyama wafugwao na wanyamapori ambapo hata wakiwa wametegwa na wao kuwategua na kuwapa matibabu.