Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, leo ameongoza zaidi ya washiriki 13,000 katika mbio za NBC Dodoma Marathon 2026 zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, huku akiipongeza Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kufanikisha ukusanyaji wa shilingi bilioni 1 zitakazotumika kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania kupitia miradi ya afya ya mama na mtoto. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa maeneo matatu muhimu ya kijamii ambayo ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua, kugharamia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo, pamoja na kuimarisha huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wanaoishi na ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell).
Mbio hizo, ambazo zimeendelea kujijengea hadhi kama moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo nchini, zilihusisha washiriki kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali, huku zikishuhudia ushindani mkubwa kati ya wanariadha wa Tanzania na Kenya katika mbio za kilomita 21 na 42. Dk. Nchemba, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi na sekta binafsi, walishiriki mbio za kilomita tano (5) kuhamasisha mazoezi na maisha yenye afya.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi na wadau wa mbio hizo, Dk. Nchemba alisema mafanikio ya NBC Dodoma Marathon yanaonesha jinsi ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unavyoweza kuleta matokeo yenye manufaa makubwa kwa jamii.
Alisema ongezeko la washiriki kutoka 1,500 mwaka 2020 hadi zaidi ya 13,000 mwaka 2026 ni ushahidi wa mwamko mkubwa wa Watanzania katika kushiriki michezo, kuzingatia afya zao na kuunga mkono shughuli za maendeleo kupitia michezo.
“NBC Dodoma Marathon imekuwa zaidi ya mashindano ya riadha. Leo ni jukwaa linalounganisha Watanzania na marafiki kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kufanya jambo kubwa zaidi—kuokoa maisha. Nawahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na figo,” alisema Dk. Nchemba.
Aidha alisema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika Jiji la Dodoma kwa kupanua na kuboresha barabara muhimu, hatua itakayorahisisha shughuli za usafirishaji na wakati huo huo kuongeza usalama wa washiriki wa mbio hizo katika miaka ijayo.
Waziri Mkuu pia aliutaka uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuendelea kuziunga mkono mbio hizo kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa jiji hilo kupitia ongezeko la wageni, shughuli za utalii wa ndani, biashara za hoteli, migahawa, usafiri na huduma nyingine zinazochochewa na tukio hilo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema NBC Dodoma Marathon imeendelea kuwa kichocheo muhimu cha uchumi wa mkoa huo kwa kuongeza mzunguko wa fedha na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa kila mwaka.
Aliishukuru Benki ya NBC kwa kuendelea kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya Mkoa wa Dodoma kupitia uwekezaji wake katika afya, michezo na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, alisema mafanikio ya mbio hizo yanaakisi dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kutumia biashara kama chachu ya kuleta maendeleo ya kijamii.
Alisema kati ya fedha zilizokusanywa, shilingi milioni 600 zimeelekezwa moja kwa moja katika utekelezaji wa malengo makuu ya NBC Dodoma Marathon kupitia taasisi tatu zinazotoa huduma muhimu za afya nchini.
Katika hafla hiyo, Dk. Nchemba na Bw. Sabi walikabidhi hundi za misaada ambapo: Shilingi milioni 200 zilikabidhiwa Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya kupanua programu ya ufadhili wa wakunga ili kuboresha huduma za afya ya uzazi, Shilingi milioni 200 zilikabidhiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kugharamia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo na Shilingi milioni 200 zilikabidhiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kusaidia huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu.
“Mafanikio haya yanatokana na dhamira yetu ya kuhakikisha mafanikio ya biashara yanaenda sambamba na ustawi wa jamii. Tunawashukuru washiriki wote, wadhamini na wadau mbalimbali waliochangia kufanikisha NBC Dodoma Marathon 2026. Ushirikiano huu umewezesha kuokoa maisha ya Watanzania wengi,” alisema Sabi.

Alitoa shukrani maalumu kwa wadhamini wakuu wa mbio hizo akiwemo Sanlam Allianz, GSM Group, Vodacom Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wadau wengine waliochangia mafanikio ya tukio hilo.
Matokeo ya Mashindano
Katika mbio za kilomita 42 (Full Marathon) kwa upande wa wanaume, mwanariadha kutoka Kenya Edwin Koech aliibuka mshindi wa kwanza kwa kutumia muda wa saa 2:05:12, akifuatiwa na Vitalis Kibiwott aliyemaliza kwa saa 2:12:18.
Kwa upande wa wanawake, Agnes Ngolo wa Kenya alitwaa ushindi kwa kutumia muda wa saa 2:32:36, huku Jacinta Chepkoech, pia kutoka Kenya, akimaliza wa pili kwa muda wa saa 2:33:26.
Washindi wa nafasi ya kwanza hadi ya kumi walizawadiwa fedha taslimu, ambapo washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake kila mmoja alijishindia Tsh milioni 11.5.
Katika mbio za kilomita 21 (Half Marathon) kwa wanaume, Bernard Geay wa Tanzania aliibuka mshindi wa kwanza kwa muda wa saa 1:02:46, akifuatiwa na Simon Kelenzoke wa Kenya (1:02:57), huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Michael Geay wa Tanzania kwa muda wa 1:02:59.
Kwa upande wa wanawake, Magdalena Shauri wa Tanzania aliibuka mshindi wa kwanza kwa muda wa 1:08:59, akifuatiwa na Doreen Chetzop wa Kenya aliyemaliza kwa muda wa 1:10:36.
Washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21 kwa wanaume na wanawake walijishindia Tsh milioni 5.5, huku washindi wa pili wakiondoka na Tsh milioni 2.5.
NBC Dodoma Marathon imeendelea kuthibitisha kuwa si tu tamasha kubwa la michezo nchini, bali pia ni jukwaa la kuhamasisha afya, kuunganisha jamii, kukuza uchumi wa Jiji la Dodoma na kuchangia moja kwa moja kuboresha huduma muhimu za afya kwa Watanzania.