OFISI ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imetangaza hafla ya uwasilishaji “Tamko la Pamoja” linalohusu mazungumzo yaliyofanyika baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT Wazalendo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Wakati wa hafla hiyo itakayofanyika Alkhamis wiki hii kwenye viwanja vya Ikulu ya Zanzibar, Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman watashuhudia uwasilishaji wa tamko hilo pamoja na kusainiwa kwa makubaliano yaliyofikiwa na vyama hivyo.
Vyama hivyo vimekuwa vikijadiliana namna ya kuondoa mkwamo wa kisiasa kufuatia madai ya ACT Wazalendo ya kuhujumiwa uchaguzi mkuu wa tarehe 28-29 Oktoba 2026 ambako CCM ilitangazwa kushinda nafasi ya urais pamoja na kujipatia wingi mkubwa wa viti vya uwakilishi, ubunge na madiwani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Raqey Mohamed, hafla hiyo inatarajiwa pia kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali zote mbili pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa, taasisi za dini na Waandishi wa Habari.
Baada ya uchaguzi mkuu, ACT Wazalendo kilikataa kushirikiana na CCM kwa ajili ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa [SUK] na kusababisha Rais Dk. Mwinyi kuunda serikali ya chama kimoja kinyume na maamuru ya Katiba ya Zanzibar.
Haijafahamika sawasawa muundo wa makubaliano yaliyofikiwa lakini inajulikana mazungumzo yaliyofanyika yaligusa maeneo ya haja ya Zanzibar kupata katiba mpya; kuangalia upya mfumo wa Government of National Unity [GNU], Tume ya Uchaguzi Zanzibar [ZEC] na Utumishi wa Umma katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.