MAHAKAMA ya Wilaya ya Simanjiro, mbele ya Onesmo Nicodemos, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya hiyo, imemhukumu, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remit, Wilaya ya Simanjiro, Godbless Felix Mollel, katika shauri la uhujumu uchumi namba 22415/2025, ambapo mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. Anaripoti Mwandishi Wetu, Simanjiro … (endelea).
Hapo awali, mshtakiwa alishtakiwa kwa makosa ya ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kikisomwa pamoja na aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupanga, Sura ya 200, Marejeo ya mwaka 2022.
Aidha, alishtakiwa kwa kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258, 265 na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka ishirini (20) gerezani kwa kosa la kwanza la ufujaji na ubadhirifu.
Katika kosa la pili la wizi akiwa mtumishi wa umma, mshtakiwa pia alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja (1) gerezani.
Hata hivyo, kwa kuwa adhabu hizo zitatumikiwa kwa pamoja, mshtakiwa atatumikia kifungo cha jumla cha miaka ishirini (20) gerezani.
Aidha, mahakama iliamuru mshtakiwa kurejesha kiasi cha shilingi 3,300,000 alichobainika kukichota katika akaunti ya Benki ya Maendeleo ya Kijiji cha Ruvu Remit.
Shauri hili liliendeshwa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Wakili Faustin Mushi.