NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Amani Golugwa amesema David Jumbe, msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amepatikana akiwa na pingu mikononi baada ya taarifa za kutoweka kwake kusambaa mitandaoni.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Golugwa amesema taarifa hizo amezipata kutoka kwa mke wa Jumbe ambaye amethibitisha kuwa mumewe amerejea nyumbani akiwa bado na pingu mikononi.
Amesema askari wa Jeshi la Polisi waliofika katika makao makuu ya Chadema leo Alhamisi 21 Mei 2026 majira ya saa tatu asubuhi walijitambulisha kuwa wanatoka Kituo cha Polisi Oysterbay na walikuwa wakimtafuta Jumbe wakidai ametoweka na pingu.
Kwa mujibu wa Golugwa, askari hao walidai kuwa Jumbe alijificha ndani ya ofisi za Chadema na walitaka kufunguliwa ili waweze kumfungua pingu hizo.
“Tunawaambia Polisi Jumbe yupo nyumbani kwake waende kumfungulia pingu,” amesema Golugwa.
Awali, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa Jumbe alichukuliwa nyumbani kwake Mabwepande, Bunju jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana.
Taarifa inayodaiwa kutolewa na mke wa Jumbe ilieleza kuwa alikuwa akirejea nyumbani na alipofika getini alifuatwa na watu hao waliomkamata na kumuingiza kwenye gari aina ya Land Cruiser kabla ya kuondoka kwa mwendo wa kasi.
Taarifa hiyo ilidai kuwa Jumbe alipiga kelele na kujaribu kujitetea lakini alizidiwa nguvu, huku majirani waliojitokeza wakijaribu kuifuatilia gari hiyo bila mafanikio.
Katika mkanganyiko huo, Jumbe anadaiwa kudondosha kiatu chake kabla ya kuondolewa na watu hao ambao hawakujitambulisha kwa familia yake.
MwanaHALISI Digital inaendelea kumsaka Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kwa ufafanuzi kuhusu tukio la kuhojiwa kwa Golugwa na madai ya kutoweka kwa David Jumbe.