BARAZA la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) limepanga kwamba Alhamisi ya tarehe 29 Oktoba 2026, itakuwa siku ya kukumbuka mauaji ya watu zaidi ya 500 yaliyotokea 29 Oktoba 2025.Anaandika Joster Mwangulumbi Dar es salaam … (endelea)
Itakuwa siku maalumu kwa ajili ya maaskofu na mapadri nchi nzima kuwafariji wafiwa, kuwajengea moyo wa subira na kuwatakia wafu wawekwe mahali pema peponi.
Watawakemea waliohusika na mauaji, waliotoa amri ya kuua na waliofyatua risasi kutekeleza amri. Watasisitiza uwajibikaji.
Watakemea nadharia kwamba watu kutoka nje ndio waliohusika na mauaji. Sina shaka hawataacha kulaani taarifa kuwa waandamanaji walikuwa na silaha.
Kuna wajinga na malofa hawajui nguvu ya Kanisa Katoliki, ujasiri wao wa kukemea maovu na ushawishi. Wakipigwa leo, wakiuawa na wakipitishwa katika mateso, wanajua ushindi unakaribia.
Hao wajinga na malofa wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kulaani uwepo wa misa ya Alhamisi wakidai ni uchochezi wa wazi na wengine wamefikia kushauri misa hiyo ifutwe kwa vile itakuwa sawa na kutonesha vidonda. Hao hawajalijua Kanisa Katoliki.
Kwa faida ya wasiojua, Kanisa Katoliki (Tanzania na duniani), hili ambalo makao yake ni Vatican katika jiji la Rome, Italia, lipo kwa ajili ya kazi tatu kubwa: Ukuhani (Priestly), Unabii (Prophetic), na Huduma (service).

Ukuhani ni kazi inayohusu kumuunganisha mwanadamu na Mungu. Katika kazi hii, Kanisa hutoa sakramenti za Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi (misa), Kitubio, Upako wa wagonjwa, Daraja Takatifu, Ndoa. Bila hizi, kwa imani ya Kikatoliki, hakuna wokovu kamili.
Kwa hiyo Kanisa huadhimisha misa kila siku kwani ndio moyo wa maisha ya Mkatoliki. Pia huombea watu: novena, maombi ya waumini na sala ya faragha.
Kuhusu unabii, hii ndiyo kazi inayomtoa askofu/ padri nje ya kanisa kwenda barabarani kupinga dhuluma. Hufundisha na kuhubiri Injili yaani hueleza mambo yaliyo mema na mabaya kulingana na Biblia.
Hapa Kanisa Katoliki husema wazi bila kupepesa macho kwamba mali ya umma ni ya wote, serikali lazima ihudumie maskini, kodi isitumike kukandamiza watu, ardhi ya asili ya watu isiporwe.
Askofu/ padri akiona watu wanafukuzwa Ngorongoro au gesi ya Mtwara inachukuliwa bila faida, kazi yake ya kinabii inamlazimisha akemee.
Kupitia unabii Kanisa hutetea utu wa binadamu. Ndiyo maana, TEC hutoa matamko kabla na baada ya kila uchaguzi, hulaani vurugu na mauaji na huweza kupinga hata kodi mpya inayotesa wananchi.
Hii siyo siasa wala si kuchanganya dini na siasa bali ni Utume.
Kazi ya tatu ya Kanisa Katoliki ni kutoa huduma kwa jamii. Kanisa lina shule na vyuo vikuu, hospitali na zahanati, miradi ya maji vijijini na kilimo.
Baadhi ya mashirika yake hujihusisha na ugawaji wa chakula wakati wa njaa, kuwatunza yatima na wazee. Kadhalika Kanisa lina Kituo cha Sheria na Haki kwa ajili ya kuwasaidia, mahakamani bila malipo, wananchi wanaonyang’anywa ardhi.
Serikali na watu wasiolijua Kanisa Katoliki wanadhani wanaweza kuliamrisha lisifanye kazi ya unabii bali ukuhani na huduma. TEC wana msimao hata pale wanapopokea vitisho au kudhuriwa.
Padri Charles Kitima, Katibu Mkuu wa TEC, alijeruhiwa vibaya Mei mwaka jana na watu wasiojulikana, lakini hakuacha unabii wala kukimbia nchi. Mapdri wengine walitekwa, wakadhalilishwa lakini waliendelea na utume wao.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000 yalipofanyika mauaji ya wafuasi kadhaa wa Chama cha Wananchi (CUF) nchini Zanzibar, pamoja na matukio ya kuchomwa makanisa 25, Kanisa Katoliki lilikemea kwa nyaraka za siri. Askofu Augustine Shao alikemea na hakukimbia nchi.
Baada ya mauaji ya watu wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025, wachungaji na maaskofu wa makanisa mengine walikimbia nchi, lakini si maaskofu wala mapadri wa Kanisa Katoliki. Tarehe 9 Novemba 2025 TEC waliandaa maombezi, hawakimbii utume.
Matatizo hulijenga Kanisa. Kwa wasiojua, baada ya Vita Kuu ya Pili, Kanisa Katoliki lilipata nguvu kubwa duniani kwa sababu tatu kuu.
Kwanza: Kanisa lilionesha ujasiri kwa kupinga utawala wa Chama cha Wafanyakazi Ujerumani (Nazi). Licha ya mapadri kadhaa kuuawa, waliosalia walipaza juu sauti zao bila woga.
Makao makuu ya Kanisa (Vatican), Papa Pius XII alikemea mauaji kwa waraka wa siri mwaka 1943 na kuokoa Wayahudi zaidi ya 400,000. Wakati makanisa mengine ya Kiprotestanti yalivunjika Ujerumani, Kanisa Katoliki liliendelea kuwepo.
Pili: Kanisa Katoliki lilikuwa kizuizi cha kuenea ukomunisti katika mataifa ya Ulaya na Asia. Mwaka 1949, Papa Pius XII alisema wazi “Ukomunisti ni adui wa Mungu na binadamu”.
Tatu: Kanisa likasaidia kujenga Umoja wa Mataifa (UN). Taarifa zilizopo zinaonesha mwaka 1945, Vatican ilikuwa mpatanishi wa kwanza wa kimataifa na ilisaidia kuundwa kwa UN.
Kwa kifupi Kanisa Katoliki baada ya vita liliamua “kulaani uovu wa chama cha Nazi na kukema ukomunisti” na ndiyo ikawa nguvu ya maadili duniani. Hata nchi za Kikomunisti kama Poland (Solidarnosc 1980s) na Ufilipino (People Power 1986) zilitumia ishara za Kikatoliki kupindua serikali.
Hapo juu nimekueleza kwamba Vatican ilisaidia kuundwa kwa UN. Vatican haikusaidia na kuondoka bali ilipewa hadhi ya kipekee; siyo kuwa mwanachama wa kudumu bali hadhi ya Mwangalizi wa Kudumu (Permanent Observer)
Ndani ya Ukumbi wa Baraza Kuu, New York, kuna kiti kimeandikwa “HOLY SEE” – sio “Vatican City”.
Holy See ndiyo jina la kidiplomasia la Kanisa.Tangu 1964 Vatican – kupitia Mwangalizi wa Kudumu – inaweza kuhudhuria mikutano yote ya Baraza Kuu, Baraza la Usalama, na mashirika ya UN. Balozi wake anaweza kuongea na kutoa maoni ila hawezi kupiga kura. Nchi ya pili kupewa hadhi hiyo ni Palestina.
Vatican ilikataa kuwa mwanachama wa kudumu kwa vile “Siyo nchi ya kawaida ya kisiasa, ni sauti ya kiroho”.
Ikiwa Vatican ingekuwa mwanachama, ingebidi ipige kura za kisiasa kuhusu mfano vita na vikwazo na hilo lingeitoa kwenye nafasi yake ya upatanishi.
Lakini ina nguvu kuliko wanachama wengi. Vativan ina balozi 183 duniani; Marekani ina 184 na Uingereza ina balozi 230. Hii inaifanya Vatican isikike kila mahali.
Katiba ya Vatican inaruhusu Papa kutuma ujumbe kwa marais 183 moja kwa moja bila kupitia UN. Mwaka 1965 Papa Paulo VI ndiye alikuwa wa kwanza kuhutubia UN ujumbe wake ulikuwa wa kupinga vita.
Mwaka 2015 na 2023, Papa Francis alihutubia tena UN kuhusu mabadiliko ya tabianchi na vita vya Ukraine.
Kwa hiyo, TEC ikiwasilisha taarifa Vatican kuhusu mauaji ya Oktoba 29, 2025, upo uwezekano wa kufika mezani kwa Katibu Mkuu wa UN kupitia balozi wa Vatican – bila hata Tanzania kuweza kuizuia. Kwa hiyo, kuhangaika na TEC ni kujisumbua.
Mwisho.
