MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche, ameitaka serikali ya Kenya kuhakikisha mwanaharakati Twaha Mwaipaya anapatikana akiwa hai na salama.Anaripoti Zakia Nanga Dar es Salaam … (Endelea)
Heche amemtaka Rais wa Kenya William Ruto, kuchukua hatua kutokana na tukio la kutekwa kwa Mwaipaya katika eneo la Kamulu, nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Akizungumza kupitia mitandao yake ya kijamii leo, 26 Oktoba 2026, Heche amesema Chadema imefanya jitihada za usiku kucha kuwasiliana na vyombo husika nchini Kenya ili kupata taarifa kuhusu aliko Mwaipaya.
Heche amesema, ingawa chama hicho hakiamini kuwa serikali ya Kenya ina sababu ya kumteka mwanaharakati huyo, kina wasiwasi kuhusu uwezekano wa watu waliohusika na tukio hilo kupata msaada wa ndani ili kutekeleza kitendo hicho.
“Usiku kucha tumejitahidi kufanya mawasiliano na vyombo vinavyohusika Kenya ili kuweza kupata taarifa ya aliko Twaha Mwaipaya. Tunajua serikali ya Kenya haina sababu ya kumteka Twaha. Lakini pia tunajua si rahisi hawa watekaji kuingia nchi nyingine na kumchukua mtu bila kusaidiwa na watu wa serikali hiyo,” amesema Heche.
Ameongeza kuwa serikali ya Rais Ruto ichukue hatua za haraka kwakuwa tukio hilo linaweza kuathiri taswira ya Kenya kimataifa, hususani katika masuala ya demokrasia na ulinzi wa haki za binadamu.
Heche amesema Kenya imekuwa ikitambulika ni nchi inayotoa nafasi kwa wanaharakati na wakosoaji wa kisiasa, hivyo tukio la mtu kutoweka kwa mazingira yanayodaiwa kuwa ya utekaji ndani ya mipaka yake linazua maswali kuhusu usalama wa watu wanaotafuta hifadhi nchini humo.
“Hili litakuwa doa kubwa sana kwa serikali ya Kenya kuruhusu watekaji kuingia na kumchukua mtu ndani ya mipaka yao. Kenya ni nchi ya kidemokrasia, kama mtu amekimbilia kwenu na kupata hifadhi hawezi kutekwa akiwa Kenya,” amesema.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo amewataka Watanzania kukataa vitendo vya ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, akidai kuwa baadhi ya watawala wanatumia vitendo vya vitisho, utekaji na kunyamazisha sauti za wanaopinga uovu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Mwaipaya anadaiwa kuchukuliwa na watu wenye silaha waliokuwa kwenye msafara wa magari matatu, yakiwemo magari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop, katika eneo la Kamulu, nje kidogo ya Nairobi.
Taarifa hiyo imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa mwanaharakati huyo na kuibua mjadala kuhusu ulinzi wa haki za binadamu, usalama wa wakimbizi wa kisiasa na ushirikiano wa kiusalama kati ya Tanzania na Kenya.
Chadema kinaendelea kusisitiza umuhimu wa kupatikana kwa Twaha Mwaipaya akiwa hai na salama, huku macho yakielekezwa kwa mamlaka za Kenya juu ya hatua zitakazochukuliwa kufuatilia tukio hilo.
Mwisho.