RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amezitaka serikali za Tanzania na Kenya kuwajibika haraka kuokana na taarifa za kutekwa kwa mwanaharakati Twaha Mwaipaya nchini Kenya.Anaripoti Zakia Nanga Dar es Salaam … (Endelea)
Mwabukusi ametoa kauli hiyo kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa tukio hilo linahitaji hatua za haraka na za wazi kutoka kwa mamlaka husika bila kuficha ukweli wala kutumia mbinu za kukwepa uwajibikaji.
Amesema utekaji ni uhalifu unaokiuka utu wa binadamu huku akisisitiza kuwa mamlaka za Kenya zina wajibu wa kisheria na kimaadili kuhakikisha usalama, uhai na utu wa Mwaipaya.
“Hivi tunatakiwa kumdai kutoka Serikali ya Kenya au Wizara yetu yenye dhamana ili kupata uwajibikaji? Utekaji ni uhalifu dhidi ya utu. Mamlaka za Kenya zina wajibu mkubwa katika kuhakikisha ulinzi wa uhai na utu wa Twaha Mwaipaya,” aliandika Mwabukusi.
Kiongozi huyo amekosoa tabia ya baadhi ya viongozi na vyombo vya dola kushughulikia matukio mazito kwa kuficha ukweli, akieleza kuwa taifa linahitaji ukweli, haki na uwajibikaji ili kurejesha imani ya wananchi katika taasisi zinazohusika.
“Ndiyo maana nasema kama taifa tunahitaji ukweli, haki na uwajibikaji. Siyo usanii na ujanja ujanja wa kufunika kombe mwanaharamu apite. Lazima tuliponye taifa kutoka katika mkwamo huu usio wa kawaida,” alisema.
Kauli ya Mwabukusi inakuja wakati tukio hilo likizua wasiwasi miongoni mwa wadau wa haki za binadamu nchini Tanzania na Kenya, huku kukiwa na wito wa mamlaka husika kutoa ufafanuzi wa wazi na kuchukua hatua zinazohitajika.
Hata hivyo, ni muhimu kwa mamlaka za nchi hizo kutoa taarifa rasmi kuhusu mazingira ya tukio hilo, hatua zilizochukuliwa na juhudi zinazoendelea kuhakikisha usalama wa Mwaipaya na kuwabaini na kuwachukulia hatua wote watakaothibitika kuhusika na uhalifu huo.
Mwisho.