BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi ya NBC Championship, imejivunia mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika mchezo wa soka nchini huku ikikabidhi kombe la ubingwa wa msimu wa 2025/2026 kwa Geita Gold FC, timu iliyotwaa taji hilo baada ya kumaliza ligi ikiwa kileleni kwa alama 77. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Ubingwa huo unaipa Geita Gold FC tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027 sambamba na Kagera Sugar FC iliyomaliza nafasi ya pili kwa alama 71 na hivyo nayo kufuzu kushiriki ligi hiyo.
Kombe hilo lilikabidhiwa jana katika Uwanja wa Nyankumbu, Geita, baada ya Geita Gold FC kuhitimisha msimu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Big Man FC ya Lindi katika mechi iliyoshuhudiwa na mamia ya mashabiki pamoja na viongozi mbalimbali wa soka, serikali na vyama vya siasa.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Biashara wa NBC Kanda ya Ziwa, Mafwimbo Bihemo, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema benki hiyo inafurahishwa na namna uwekezaji wake katika soka unavyoendelea kuzaa matokeo chanya kupitia ongezeko la ushindani, kuibuka kwa vipaji vipya na kuimarika kwa viwango vya ligi za ndani.
Alisema NBC, ambayo imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 32 katika udhamini wa Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na Ligi ya Vijana, itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha soka linaendelea kukua na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

“Tunawapongeza washiriki wote wa NBC Championship kwa ushindani mkubwa waliouonyesha msimu mzima. Kipekee tunawapongeza Geita Gold FC kwa kutwaa ubingwa na Kagera Sugar FC kwa kufuzu Ligi Kuu ya NBC. Mafanikio haya yanaonyesha kiwango kikubwa cha ushindani kinachoendelea kujengeka katika soka la Tanzania,” alisema Bihemo.
Alisema NBC inaona matokeo ya uwekezaji huo kupitia maendeleo yanayoonekana katika ligi za ndani, kuimarika kwa ushindani wa vilabu na mafanikio yanayozidi kupatikana kwa timu za taifa katika mashindano ya kimataifa.
“Tunajivunia kuona soka la Tanzania likiendelea kupiga hatua. Ushindani unaoanzia ligi za vijana, NBC Championship hadi Ligi Kuu ya NBC umeendelea kuongeza ubora wa mchezo na kuzalisha wachezaji wenye uwezo wa kushindana katika viwango vya juu zaidi. Haya ndiyo matokeo tunayolenga kuyaona kupitia uwekezaji wetu,” aliongeza.
Bihemo alisema NBC itaendelea kuboresha mchango wake kwa wadau wa soka kupitia huduma mbalimbali za kifedha zikiwemo mikopo kwa vilabu, bima za afya kwa wachezaji na benchi la ufundi pamoja na elimu ya fedha inayolenga kuimarisha ustawi wa wadau wa mchezo huo.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliipongeza NBC kwa mchango wake mkubwa katika kukuza soka la Tanzania kupitia udhamini wa ligi hizo tatu, akibainisha kuwa ushindani wa sasa katika ligi za ndani ni miongoni mwa matokeo makubwa ya uwekezaji huo.
“Leo tunaona NBC Championship ikiwa na ushindani mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa msimu. Vilabu vinaendesha shughuli zake kwa weledi zaidi, vina uwezo wa kusajili wachezaji bora na kujiandaa vizuri kwa mashindano. Haya ni maendeleo makubwa kwa soka letu,” alisema Karia.
Aliwataka Geita Gold FC na Kagera Sugar FC kutumia fursa ya kupanda Ligi Kuu ya NBC kujiimarisha zaidi ili kuongeza ushindani katika ligi hiyo pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya viwanja ili mashabiki wao waweze kufurahia mechi za nyumbani katika mazingira bora.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa Geita Gold FC, nahodha wa timu hiyo Yusuph Mhilu aliwashukuru mashabiki, viongozi, benchi la ufundi na wadhamini kwa mchango wao katika kufanikisha ubingwa huo.
Alisema timu hiyo inatambua ushindani mkubwa uliopo katika Ligi Kuu ya NBC na tayari imeanza maandalizi ya kuhakikisha inakwenda kutoa ushindani wa kiwango cha juu msimu ujao.