JESHI la Polisi Tanzania limesema linaendelea kufuatilia kwa karibu Watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa Nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Hayo yamebainishwa leo 19 Juni 2026 na Msemaji wa Jeshi hilo, DCP David Misime ambapo amesema uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya Watu ambao awali walikuwa wakihamasisha maandamano ya 7 Julai sasa wanatumia majukwaa ya mtandaoni kuhamasishana kufanya vitendo vya kihalifu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya vitendo vinavyodaiwa kuhamasishwa ni pamoja na kufunga barabara, kuchoma shule, kuharibu mali za umma na binafsi, kushambulia Wananchi pamoja na kuvamia Askari wa Vyombo vya Ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha.
“Jeshi linawahakikishia Wananchi kuwa hali ya usalama Nchini inaendelea kuwa shwari na kwamba litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na utulivu Nchini,”. Amesema DCP Misime.