WANANCHI mbalimbali kutoka jijini Dodoma na nje ya jiji hilo wanaendelea kutembelea Banda la Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala huo katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Miongoni mwa waliotembelea banda la TARURA ni Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Ramadhani Kailima ambaye ameonesha kufurahishwa na ushiriki wa TARURA katika maonesho hayo kwani yanatoa nafasi kwa wananchi ya kupata elimu na kiwasilisha malalamiko, kero na maoni mbalimbali kuhusu barabara za Wilaya zinazosimamiwa na wakala hiyo.
Wananchi wengi waliotembelea banda la TARURA wameonyesha kuridhishwa na hali ya mtandao wa barabara kwa sasa kwani kwa kiasi kikubwa unapitika katika nyakati zote na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Evance Wilhemu mkazi wa Ntyuka jijini Dodoma ambaye ametembelea banda la TARURA ametoa ushuhuda wa jinsi TARURA ilivyowasaidia kukwamua mawasiliano katika eneo lao kwa kuwajengea daraja la mawe eneo la Ntyuka machinjioni.
“Kabla ya ujenzi wa daraja la mawe, barabara ilikuwa haipitiki kabisa hususani watu wenye vyombo vya usafiri ambapo walilazimika kuzunguka umbali mrefu ili waweze kufika kwenye makazi yao lakini baada ya TARURA kutujengea daraja sasa hivi njia inapitika vizuri na kwa ujumla wananchi wamefurahi sana na tunaipongeza TARURA.” amesema Wilhemu.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu yameanza Juni 16, 2026 na yanatarajiwa kutamatika Juni 23, 2026 huku yakibeba kauli mbiu inayosema “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma endelevu”.