Dar es Salaam: MSIMAMIZI wa tanki la mafuta ghafi, Kassim Kongwa na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa kesi ya Uhujumu yenye mashtaka matatu, limo la wizi wa lita 2,800 za mafuta ya ghafi mali ya kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Limited.Anaripoti Erasto Masalu, Dar es Salaam ….(endelea).
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Juni 16, 2026 na wakili wa serikali Winiwa Kasala imewataja washtakiwa wengine kuwa ni Hassan Kimoge, Juma Issah, Halfan Halfan maarufu kama Ruba, Maria Gulaba wote ni ma opereta wa kiwanda hicho, Hemed Abdalah kibarua wa Kampuni ya Azania na mlinzi Jafar Molel.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Anna Magutu imedaiwa kati ya Juni 2 na 4, 2026 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa na nia ovu waliongoza genge la uharifu na kuiba mafuta ghafi mali ya kampuni ya Mkoani Edible Oil and Detergents Ltd.

Imeendelea kudaiwa kuwa katika tarehe hizo huko Temeke katika mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke, washtakiwa waliiba lita 2800 za mafuta ghafi yenye thamani ya sh milioni 26, mali ya kampuni hiyo.
Aidha katika shtaka la utakatishaji washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi lita 2800 za mafuta huku wakijua kuwa mafuta hayo nu zao la kosa tangulizi la wizi.
Hata hivyo washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi ambazo kwa kawaida kusikilizwa mahakama Kuu au kwa kibali maalumu kutoka kwa DPP
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi Juni 30,2026 itakapotajwa tena, washtakiwa wote wamepelekwa mahabusu kwasababu shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana.
mwisho