ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Said Issa Mohammed amesema kuwa Kamati Tendaji ya Kanda ya Pemba haina mamlaka ya kufanya uamuzi wa kumfuta uanachama.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Digital, Said Issa, amesema pamoja na Kamati hiyo kukosa mamlaka kisheria lakini pia wamekiuka katiba ya chama hicho.
“Katiba imekiukwa ilitakiwa niitwe na Mamlaka husika nisomewe tuhuma zangu, nipewe nafasi ya kusikilizwa kisha ndio utoke uamuzi lakini vipengele vyote hivyo vimerukwa,” amesema Said Issa.
Jana tarehe 7 Juni 2026, Abdullah Hassan Katibu wa Chadema, Kanda hiyo kupitia taarifa yake kwa umma amesema kuwa kamati hiyo imeketi tarehe 6 Juni 2026, kwenye ukumbi wa Pride ulikuwepo Chakechake visiwani humo.
Hassan alisema kuwa kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa kanda hiyo, Omar Nassor kilijadili mwenendo wa Said Issa na kubaini kuwa ni kinyume na chama hicho.
“Tunautaarifu umma kuanzia tarehe 6 Juni Saidi Issa Mohammed si mwanachama na wala hatambuliki kama kiongozi au mwakilishi wa chama katika ngazi yoyote .
“Hivyo kauli, matendo au shughuli zozote atakozozifanya baada ya tarehe hiyo zitakuwa ni za kwake binafsi na hazitahusishwa na chama.
Hata hivyo Katiba ya Chadema inaeleza kuwa mwanachama yoyote atakayekishtaki chama atakuwa amejivua uanachama yeye mwenyewe.