WATU sita wakiongozwa na mfanyabiashara Gilbert Nyamitah wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka 28 ikiwemo uhujumu uchumi na utakatishaji wa zaidi ya shilingi milioni 355.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Washtakiwa wengine ni Fabian Kulwa, Mnyamisi Selumamala, Salum Kapene, Onesmo Aron na Joram Fanuel.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki 4 Mei 2026 Wakili wa Serikali Michael Sindai alidai kuwa kati ya Mei 2025 na Aprili 2026, washtakiwa waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine pamoja na matumizi mabaya ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) vya watu wengine kusajili laini za simu.
Aidha, Nyamitah na Kulwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo wakijua zimetokana na shughuli haramu.
Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Kesi imeahirishwa hadi 18 Mei 2026.
Nyamitah na Kulwa wamepelekwa mahabusu kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana, huku washtakiwa wengine wakisubiri kutimiza masharti ya dhamana.