RAIS wa Jumuiya ya Wanafunzi wa elimu ya Juu nchini Tanzania TAHLISO Geofrey Kiliba amelitaka Jeshi la Polisi Nchini Tanzania kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuweza kubaini ukweli kuhusu kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) James Temba aliyeuwawa na kisha mwili wake kutupwa katika Mto Msimbazi, eneo la Baracuda, Jijini Dar Es Salaam.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Katika chapisho lake la salamu za pole leo Jumanne 5 Mei 2026, Kiliba amesema tukio hilo limegusa mioyo ya wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu Nchini na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa Jumuiya ya TAHLISO inalichukua tukio hilo kwa uzito mkubwa, akitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na wanafunzi wa IFM.
“Kwaniaba ya Jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi za elimu ya juu Tanzania (TAHLISO), ninaliomba Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na wa haraka ili kusudi wahusika wa tukio hili wabainike na kufikishwa mbele ya Vyombo vya sheria.” Ameandika Kiliba.
Katika hatua nyingine Kiliba amewasihi wananchi wote kutoa ushirikiano wa dhati kwa Vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa zitakazoweza kusaidia kufanikisha uchunguzi juu ya tukio hilo la mauaji.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tayari limetangaza kuanza uchunguzi wa kina kufuatia kuuwawa kwa James Temba, mkazi wa Tabata Chang’ombe, Polisi walikaririwa wakisema kwamba wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kifo hicho na kuwabaini wahusika.