JESHI la Polisi Tanzania limeonya watu au vikundi vinavyowazuia madereva wa mabasi na malori kuendelea na safari, likisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya hivyo.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Jumanne 29 Septemba 2026, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Awadh Juma, amesema kuzuia vyombo vya usafiri au kuwafanyia hujuma madereva ni kinyume cha sheria.
CP Awadh pia amesema mfumo wa pointi za leseni bado haujaanza kutumika, akiwataka madereva na wananchi kutopuuzia taarifa zisizo rasmi zinazosambazwa mitandaoni.
Kauli hiyo imekuja wakati huduma za usafiri zikisuasua katika baadhi ya mikoa. Madereva katika vituo vya mabasi vya Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam wameripotiwa kusitisha safari wakilalamikia kukamatwa kwa magari, kufungiwa leseni na masuala yanayohusiana na mfumo wa pointi.
Hali hiyo imesababisha abiria kukwama katika vituo mbalimbali, huku Polisi ikisema inaendelea kufuatilia hali hiyo na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.