WATU wanane wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya basi la abiria kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Kijiji cha Chumbi, Kata ya Chumbi, Tarafa ya Mohoro wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, ajali hiyo imetokea 22 Septemba 2026, majira ya saa 9:15 mchana katika barabara kuu ya Lindi–Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa basi lenye namba za usajili T930 ERF, aina ya Toyota Coaster, lililokuwa likitokea Mohoro kuelekea Dar es Salaam, liligongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T511 EPS, likiwa na tela lenye namba T469 EPL, aina ya Scania.
Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Halfan Cosmas Madodo (44), mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, huku lori likiendeshwa na Hassan Salum Goro (30), mkazi wa Dodoma.
Polisi imesema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu wanane waliokuwa ndani ya basi hilo, wakiwemo dereva, kondakta na abiria.
Majeruhi 12 wamepatikana, ambapo wanane wamefahamika na wengine wanne bado hawajatambuliwa. Baadhi ya majeruhi wamepatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Muhoro, huku wengine wakipelekwa katika hospitali kubwa kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa ni uzembe wa dereva wa basi hilo, ambaye alishindwa kulimudu gari na kuhama upande wa kulia wa barabara kabla ya kugongana uso kwa uso na lori.
Miili ya waliofariki imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Muhoro kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limetoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali na madhara kwa watumiaji wa barabara.