WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kutumia fursa zilizopo kuunganisha nguvu zao na kushirikiana ili kupigania ustawi wa maisha yao na taaluma yao mbele ya waajiri wao. Anaripoti Mwandshi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), katika mafunzo kuhusu fidia kwa wafanyakazi yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Nyamhokya, amesema kuwa bila umoja na ushirikiano ni vigumu sauti za wanahabari kusikika kwa uzito unaostahili na hivyo kukosa msukumo mkubwa kwa serikali na waajiri wao.
“TUCTA tunafarijika sana JOWUTA kujiunga nasi, tunawaahidi kushirikiana naye bega kwa bega kwa kuwa ni watu muhimu kwenye maendeleo ya nchi yetu. Nawaomba mshirikiane na serikali katika kutatua matatizo yanayokabili sekta yenu ikiwemo ukosefu wa mikataba kwa wafanyakazi. Nguvu yetu ni umoja, tusikubali kutenganishwa,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Mussa Juma amesema idadi kubwa ya waandishi wa habari nchini wanafanya kazi bila mikataba ya ajira iwe za kudumu au muda jambo linalowakosesha huduma muhimu za hifadhi ya jamii na fidia wanapopatwa na madhara.
“Zaidi ya asilimia 70 ya wanahabari nchini hawana ajira rasmi hivyo wanafanya kazi katika mazingira magumu yanayopunguza utulivu wao kazini. Nawaomba tushirikiane na wenzetu wa WCF na TUCTA kuboresha mazingira yetu kazini na kudai haki zetu,” amesema.
Juma amesema wamezungumza na Ofisi ya Waziri Mkuu (Wizara ya Kazi) na Kamishna wa Kazi juu ya namna bora ya kutatua tatizo la waajiri wasiowapa mikataba ya ajira waandishi wa habari.
“Siku chache zijazo serikali imetuahidi kwa kushirikiana nasi kuanza msako maalumu katika vyombo vya habari ili kubaini waajiri wanaokiuka sheria za kazi ikiwemo kutowapatia mikataba ya ajira waandishi wa habari,” amesema.
Juma amesema JOWUTA itaendelea kudumisha mshikamano ndani na nje ya tasnia ya habari ili kuhakikisha masilahi na haki za mfanyakazi zinalindwa.

Amesema uandaaji wa mafunzo ya masuala ya fidia kwa wafanyakazi yaliyotolewa kwa wanachama wa JOWUTA ni ishara ya uhusiano mwema na WCF.
” WCF wametuongezea maarifa yatakayotusaidia kwenye kazi zetu lakini pia katika maisha yetu kwa kuwa yatusaidia kuwahimiza waajiri wajiunge na mfuko huu” amesema.
Naye Mkuu wa kitengo cha mahusiano kwa umma Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi(WCF) RAULA Kunenge amesema mfuko huo utaendelea kutoa elimu kwa wanahabari na wafanyakazi wengine kuhusu haki zao wanapopata ajali au madhara yanayotokana na kazi wanazozifanya.
Amesema wanahabari ni wadau muhimu katika kufikisha elimu kwa jamii, hivyo ushirikiano kati ya WCF na JOWUTA utasaidia wananchi wengi kuelewa umuhimu wa mfuko huo na huduma zinazotolewa kwa wafanyakazi nchini.
Katika mafunzo hayo, washiriki walipata elimu kuhusu haki za wafanyakazi, umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi pamoja na namna ya kupata huduma za fidia kupitia WCF wanapopatwa na madhara yanayotokana na kazi zao.